NA ABRAHAM NTAMBARA
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli, amewaahidi wananchi wa Kata Mpya ya Ngereyani kuwa Serikali itaweka mpango wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha kata hiyo katika Bajeti ya mwaka ujao wa 2026/2027.
Ahadi hiyo imetolewa leo Januari 13, 2026, wakati Mhe. Kalli alipokuwa akisikiliza na kutatua kero za wananchi hao, ambao waliomba kujengewa Kituo cha Afya ili waepukane na adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.
“Mambo mengi mazuri mmeyasema hapa, na nitayachukua kuyafanyia kazi. Kwa kuzingatia mapenzi ya wananchi na idadi kubwa ya watu katika kata hii, kwenye bajeti ijayo ya mwaka 2026/2027 tutatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya,” amesema Mhe. Kalli.
Ameeleza kuwa, kituo hicho kikijengwa kitaweza kuhudumia pia wananchi wa maeneo ya jirani.
Aidha, Mhe. Kalli amebainisha kuwa kutokana na Kata ya Ngereyani kuwa mpya, Serikali imedhamiria kupeleka maendeleo makubwa na ya haraka, ikiwemo kuhakikisha vitongoji vyote vinafikiwa na nishati ya umeme.
Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara ili kuhakikisha zinapitika wakati wote wa mwaka.
Kuhusu huduma ya maji, DC Kalli amesema mradi mkubwa wa maji wa Tingatinga–Ngereyani wenye thamani ya shilingi bilioni 1.7 unaendelea kutekelezwa, na lengo lake ni kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi na mifugo yao mara utakapokamilika.
“Tuna mradi wa shilingi bilioni 1.7 na mkandarasi yupo kazini. Tunataka ukikamilika kusiwe na mgao wa maji, bali yapatikane kwa saa 24. Kila mradi wa maji tunaoutekeleza lazima tuweke tawi maalum kwa ajili ya mifugo, kwa sababu mifugo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wenu,” ameongeza DC Kalli.
Katika hatua nyingine, DC Kalli ametoa rai kwa viongozi wa kata hiyo kuhakikisha maendeleo yanajengwa kwa mpangilio mzuri, akisisitiza umuhimu wa kutenga maeneo ya barabara na mitaa wakati wa ujenzi wa makazi, ili kata hiyo iwe na mwonekano mzuri na kuepuka ujenzi holela.
Katika hatua nyingine, wananchi wa Ngereyani wameomba Shule ya Msingi Ngereyani iwe ya bweni ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kwenda na kutoka shuleni. DC Kalli ameahidi kulifanyia kazi ombi hilo.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: +255 272 970 793/ 94
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.