NA ABRAHAM NTAMBARA
Halmashauri ya Wilaya ya Longido imejipanga kuhakikisha wanafunzi wa Kidato cha Kwanza, Awali na Darasa la Kwanza walioandikishwa kwa muhula wa masomo wa mwaka 2026 wanaanza masomo pindi shule zitakapofunguliwa rasmi Januari 13, 2026.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Mhe. Thomas Ngobei, alipokuwa akizungumza baada ya kukamilika kwa ziara ya siku mbili ya kukagua maandalizi ya upokeaji wa wanafunzi hao, hususan katika shule mpya wilayani humo. Ziara hiyo ilianza Desemba 30 na kukamilika leo Desemba 31, 2025.
Amesema kuwa maandalizi yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika yanatoa matumaini kuwa ifikapo Januari 13, 2026, wanafunzi wote wanaostahili kuanza masomo kwa muhula wa mwaka 2026 wataanza masomo yao bila vikwazo vyovyote.
Kutokana na hali hiyo, Mhe. Ngobei amewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanaripoti shuleni mara shule zitakapofunguliwa, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wazazi watakaokaidi agizo hilo.
“Tumetembelea shule mbalimbali na kuhakiki maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi kwa mwaka 2026. Longido tumejipanga na tupo tayari kwa mapokezi ya wanafunzi,” amesema Mhe. Ngobei.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Afya na Maji, Mhe. Obedy Mollel, amesema kuwa baada ya kutembelea shule hizo, kamati imeridhika na maandalizi yaliyofanyika, kwani wakuu wa shule wamewahakikishia kuwa wako tayari kupokea wanafunzi wote.
“Tumejiridhisha kuwa shule zote tulizotembelea zimejipanga vizuri kwa mapokezi ya wanafunzi. Walimu wakuu wametuhakikishia kuwa wanafunzi wote watapokelewa na kuendelea na masomo yao,” amesema Mhe. Mollel.
Aidha, amewapongeza wananchi kwa kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa kata na vijiji katika kutatua baadhi ya changamoto, ikiwemo kuchangia mahitaji mbalimbali kama vile viti, meza na vitanda, ili kuweka mazingira rafiki ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Mhe. Peter Lekaneti, amewahimiza wananchi kuendelea kutatua changamoto zinapojitokeza kwa kushirikiana na Serikali, ambayo itaendelea kuongeza nguvu ili kukamilisha utatuzi wa changamoto hizo.
Mhe. Ngobei alikagua maandalizi katika Shule Shikizi ya Laalaroi na Shule ya Sekondari Noondoto, zote zilizopo Kata ya Noondoto. Aidha, alitembelea Shule ya Sekondari Mundarara na Shule ya Msingi Lesing’ita, zilizopo Kata ya Mundarara.
Alitembelea pia Shule ya Sekondari Kimokouwa, Shule ya Sekondari Kamwanga, Shule ya Msingi Kamwanga, Shule ya Sekondari Sinya, Shule ya Msingi Sinya, Shule ya Sekondari ya Wasichana Longido Samia pamoja na Shule ya Msingi Oltepes.
Katika ziara hiyo, Mhe. Ngobei aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Peter Lekaneti; Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Mhe. Obedy Mollel; Kaimu Afisa Elimu Sekondari, Bw. Mgonza Salehe; pamoja na Kaimu Afisa Elimu Msingi, Bw. Mustafa Kaisi.
Kwa mujibu wa ratiba ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, shule za Awali, Msingi na Sekondari zinatarajiwa kufunguliwa rasmi Januari 13, 2026.
Arusha- Namanga Road, Longido Town
Postal Address: S.L.P 84 Longido Arusha
Telephone: +255 272 970 793/ 94
Mobile: 0756395889
Email: ded@longidodc.go.tz
Copyright ©2016 Longido DC . All rights reserved.